24/11/2022 Madaktari wazawa mabingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kubadilisha sehemu ya mshipa mkubwa wa damu (Aorta) ambao unatoka kwenye moyo mpaka sehemu inayotoa matawi ya mishipa inayopeleka damu kwenye kichwa na ubongo (ascending aorta and arch).
Upasuaji huo unaojulikana kwa jina la kitaalamu la Bental Procedure and hemi-arch aortic repair ulichukua masaa kumi kukamilika kutokana na mshipa wa mgonjwa kutanuka ukihusisha na mshipa unaopeleka damu kwenye kichwa na ubongo.
Mbali na kuusimamisha moyo kutokana na upasuaji huo kuhusisha sehemu ya Aorta inayotoa mishipa ya damu kupeleka kwenye ubongo ilibidi wataalam hao kusimamisha msukumo wote wa damu kwenda kwenye ubongo na mwili mzima kwa muda wa dakika 45 ( Deep hypothermia and circulatory arrest).
Akizungumzia kuhusu upasuaji huo Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI Evarist Nyawawa alisema baada ya kumfanyia vipimo mgonjwa huyo waligundua kuwa valvu inayopitisha damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mshipa mkubwa na kusambaza damu mwilini (Aortic Valve) ulikuwa unavujisha damu.
Dkt. Nyawawa alisema wataalam walishauri mgonjwa huyo afanyiwe kipimo cha CT Scan ili kuchunguza mshipa wa aorta kwa kutumia kipimo kinachoitwa CT Angiograph na kuthibitisha kuwa mshipa mkubwa wa damu ulikuwa umetanuka kwa kiwango kikubwa kutoka kwenye valvu kwenda mpaka kwenye ascending aorta na sehemu ya arch of aorta.
“Tulipokea mgonjwa ambaye alikuwa na tatizo la kuumwa kifua na kubanwa kifua huku akijisikia mwili kuchoka sana hivyo kumfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO Cardiograph) na kugundua kuwa valvu inayopitisha damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mshipa mkubwa na kusambaza damu mwili mzima (Aortic Valve) ulikuWa unavujisha damu,” alisema Dkt. Nyawawa.
Dkt.Nyawawa alisema kwa kawaida mgonjwa akiwa na mshipa uliotanuka hadi kwenye arch of aorta upasuaji wake unakuwa mgumu na wa hatari kwa sababu mbali na kuusimamisha moyo unahitaji vilevile wakati wa upasuaji usimamishe msukumo wote wa damu kwenda kwenye ubongo na mwili mzima.
“Tumefanikiwa kupandikiza mshipa bandia sehemu ambayo mshipa wake ulikuwa umetanuka na kubadilisha valvu lakini pia tulitoa ile mishipa midogo midogo ya moyo (Coronary) ambayo inapeleka damu kwenye misuli ya moyo na baadaye kuipandiza tena kwenye ule mshipa bandia,” alisema Dkt. Nyawawa.
Dkt. Nyawawa alisema baada ya upasuaji mgonjwa amepona na ataweza kufanya kazi zake zote bila ya kupata dalili alizokuwa nazo hapo awali za kuchoka, maumivu ya kifua na kushindwa kupumua.
“Wagonjwa wanaopata dalili za kuchoka, pumzi kukata na kifua kubana wanapaswa kupumzika kwanza na kufika hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili waweze kupatiwa matibabu mapema kwani ni hatari mshipa wa damu mkubwa ukitanuka na kupasuka husababisha mgonjwa kupoteza maisha yake,”.
“Kuna sababu nyingi zinazosababisha mshipa mkubwa wa damu kutanuka na kupasuka lakini sababu kubwa huwa ni shinikizo la damu kwani wagonjwa wengi tuliowaona wamepata tatizo hili kutokana na kuwa na shinikizo la damu,”alisema Dkt. Nyawawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema JKCI kwa kutumia madaktari wazawa imefanikiwa kufanya upasuaji huo mkubwa kwa wagonjwa wawili ndani ya wiki moja mafanikio makubwa ambapo tofauti yao mgonjwa mmoja mshipa wake ulikuwa umetanuka sana hadi sehemu ambapo kuna mishipa midogo inayopeleka damu kwenye ubongo.
Dkt. Anjela alisema upasuaji huo unatakiwa kufanyika kwa uangalifu mkubwa kwasababu mishipa midogo ya damu isipopandikizwa vizuri mgonjwa anaweza kupata matatizo kwenye ubongo, sehemu zote za kichwa pamoja na mishipa ya damu.
“Mgonjwa mwingine tuliyemfanyia upasuaji wa aina hii alikuwa na umri wa miaka 35 ambaye mshipa wake mkubwa wa moyo ulikuwa umetanuka sana na kuchanika kwa ndani hivyo kutengeneza njia mbili kubwa ambazo zimekuwa zikipitisha damu na kuathiri mishipa ya kupeleka damu katika kichwa na ubongo,” alisema Dkt. Angela.
Dkt. Anjela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi alitoa wito kwa wagonjwa wanaopata maumivu ya ghafla ya kifua au kupoteza fahamu waende hospitali haraka kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi pamoja na kupata matibabu.
Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo Mohamed Dinya alisema amefarijika kuona wataalam wa JKCI wana utaalam mkubwa kwani hakutegemea kama angefanyiwa upasuaji huo kutokana na hali yake ilivyokuwa hivyo kuwafanya wataalam wageni waliofika katika Taasisi hiyo kuhairisha upasuaji zaidi ya mara mbili.
“Hivi karibuni kulikuwa na wataalam wa afya kutoka nchi tofauti na hapa ambao walinifanyia uchunguzi na kuondoka bila ya kunifanyia upasuaji kutokana na upasuaji wangu kuwa mgumu na wa hatari lakini madaktari hawa wa JKCI hawakukata tamaa wakasema watanifanyia upasuaji na leo kama unavyoniona naendelea vizuri,”.
“Madaktari wa hapa ni wazuri sana, watanzania wenzangu msiogope kupatiwa matibabu hapa na kukimbilia nje ya nchi kwani labda leo ningeenda nje ya nchi nisingefanyiwa upasuaji kutokana na tatizo langu kuwa kubwa na wataalam kuogopa kunifanyia upasuaji huo,” alisema Dinya.
Habari kamili na Ally Thabit