Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo ametembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road na kuzungumza na baadhi ya watumishi, huku akiupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kusimamia vizuri pesa zinazotolewa na serikali kwaajili ya miradi mbalimbali.
Dkt. Mollel amesisitiza kuwa ujenzi wa jengo mfano la Cyclotron ukiliangalia kwa nje unaweza Sema limegharimu kiasi kidogo sana cha pesa ila kwa ndani ndio utagundua thamani ya pesa iliyotumika kuwa inaendana na ubora na umadhubuti wa jengo lenyewe.
Dkt. Mollel ameomba uharaka wa umaliziaji wa jengo hilo ufanyike kwani watanzania wanahitaji huduma zake mapema iwezekanavyo huku serikali ikitaka uwekezaji wake uanze kuleta tija kwa wananchi.
Nae mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage, amemhakikishia Dkt. Mollel kumalizika mapema kwa ujenzi huo kwani kwa upande wa jengo limekamilika kwa Asilimia tisini na nane wakati mashine tayari zimekwishasimikwa kwa asilimia Mia moja huku ukisubiriwa utaratibu wa kuunganisha umeme pekee ili mashine hizo zianze kutumika kama inavyotakiwa.
Jengo hilo limekusanya mashine mbili kubwa ambazo ni PET-CT SCAN pamoja na CYCLOTRON (kiwanda cha kutengeneza mionzi) ambapo kwa sasa kwa Tanzania nzima kitakuwa ni kimoja tu, ambacho kitakuwa kikitengeneza mionzi ambayo itatumika kwa Taasisi huku mingine ikipelekwa kwenye hospitali nyingine kwaajili ya kusaidia wahanga wa huko. Kwa sasa Taasisi inanunua mionzi hiyo kutoka Afrika ya Kusini huku gharama zake zikiwa kubwa mno ukilinganisha na uwezo wa watanzania wenyewe, hivyo kukamilika kwa usimikaji huo kutakuwa msaada mkubwa sana kwa Tanzania na Afrika mashariki na kati kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment