Wednesday, 8 March 2023

Dkt. Kisenge awataka wafanyakazi wa JKCI kuwafundisha wataalamu wa afya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo

 Dkt. Kisenge awataka wafanyakazi wa JKCI kuwafundisha wataalamu wa afya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

6/3/2023 Wataalamu  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuwafundisha jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo wahudumu wa afya wa hospitali mbalimbali hapa nchini ili huduma hiyo iweze kupatikana katika maeneo mengi zaidi.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema ni jukumu la Taasisi hiyo kuhakikisha ujuzi waliokuwa nao wataalamu wake wa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo unawafikia wataalamu wengi zaidi nchini  jambo ambalo litasababisha wananchi wengi kufikiwa na huduma hiyo.

“Leo hii mtaalamu wa magonjwa ya moyo unaweza kupata tatizo la moyo ukiwa nje ya Dar es Salaam au kijini kwenu ulikozaliwa na unaweza kufa kwa kukosa huduma ya kibingwa kwa kuwa mahali ulipo haipatikani, lakini kama tutawafundisha wataalamu wenzetu jinsi ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo na huduma hii ikapatikana katika Hospitali zote itasaidia kila mgonjwa kupata huduma kwa wakati”.

“Katika Taasisi yetu tumejipanga kila mfanyakazi kuanzia mlinzi hadi wakurugenzi ambao siyo wa kada ya afya kupewa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya mtu aliyepata tatizo la dharura la kiafya ninaamini kwa kuwapatia mafunzo haya kutawasaidia kuokoa maisha ya watu watakaopata matatizo ya dharura ya kiafya mahali popote pale watakapokuwa”,alisema Dkt. Kisenge.

 Aidha Dkt. Kisenge aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa baraza hilo kwa utendaji wa kazi wanaoufanya na kuwataka kuendelea kuwahudumia watanzania wenye matatatizo ya moyo huku wakifuata mpango mkakati wa Taasisi hiyo kwa mwaka 2022/23 – 2025/26  kwa kutimiza malengo waliyojiwekea.

Dkt. Kisenge alishukuru, “Ninawashukuru wafanyakazi wa Taasisi hii kwa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ninawaomba tuendelee kushikamana kwa kufuata dira ya JKCI ili iwe taasisi ya Kimataifa”, .

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa Dkt. Janeth Madete aliwapongeza viongozi wa baraza hilo kwa kuongoza kikao vizuri na kujadili mambo mbalimbali ya kazi za Taasisi hiyo kwa faida ya watanzania.

Dkt. Janeth alisema kuwepo kwake katika kikao hicho alijifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna wajumbe wa baraza hilo walivyojadili kwa pamoja jinsi ya kutoa huduma bora kwa wananchi wakiwemo wagonjwa.

“Nimeona hapa mmejadili maslahi ya wafanyakazi wakiwemo wa chini ambao mishahara yao ni midogo, ninaupongeza uongozi wa JKCI kwa kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa chini kwa kufanya hivi utendaji kazi wa Taasisi hii utaenda vizuri”, alipongeza Dkt. Janeth.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment