TAARIFA KWA UMMA |
UPATIKANAJI WA GESI
ASILIA KWA MATUMIZI YA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM
Kumekuwepo
na mwitikio mkubwa wa Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka mfumo ya gesi
asilia (CNG) kwenye magari yao ili kuweza kupunguza gharama ya uendeshaji wa
magari. Watumiaji wa gesi asilia kwenye magari wanaweza kuokoa hadi zaidi ya
asilimia 45 ya gharama ya matumizi ya mafuta.
Mpaka
sasa, tunavyo vituo viwili katika mkoa wa Dar es Salaam kikiwemo cha Ubungo
kinachomilikiwa kwa Ubia kati ya TPDC na PANAFRICA na kile kinachomilikiwa na
Anric kilichopo Tazara. Lakini pia, Kampuni ya Dangote inamiliki kituo binafsi
kilichopo Mtwara. Vituo vingi zaidi vinahitajika ili kukidhi mahitaji
yaliyoongezaka kwa wingi katika muda mfupi.
Jumla
ya vituo 9 vya kujaza gesi kwenye magari vinatarajiwa kujengwa na kukamilka
ndani ya miezi 24 ijayo, ambapo;
- Vituo viwili vya kujaza gesi kwenye
magari vitapatikana kabla ya mwisho wa mwaka huu. Vituo hivyo vinajengwa
na kampuni ya TAQA DALBIT katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na kituo
kingine kitajengwa Sinza mkabala na barabara ya Sam Nujoma. Vituo hivi
vitakuwa na karakana za kuweka mifumo ya CNG kwenye magari. Aidha, vifaa
vya kujenga vituo hivi tayari vimeanza kusafirishwa kuja nchini.
- Kituo Kikuu (Mother Station) cha TPDC
kitajengwa Mlimani City barabara ya Sam Nujoma. Kituo hiki kitakuwa na
uwezo wa kujaza magari sita kwa wakati mmoja pamoja na malori sita ya
kubeba CNG kupeleka kwenye vituo vidogo. Kituo mama hicho kitaweza
kuongeza kasi ya uwepo wa vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari.
Kituo hiki pia kitakuwa na Karakana ya uwekaji wa mifumo ya gesi kwenye
magari itakayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mkandarasi wa
ujenzi wa kituo hiki ameshapatikana.
- Vituo vingine vitakavyojengwa katika
kipindi cha miezi 24 ni pamoja na; kituo kitakachojengwa Bagamoyo na
kampuni ya TURKY Petroleum, kituo kitakachojengwa na Kampuni ya Anric huko
Mkuranga, kituo kitakachojengwa na Kampuni ya BQ katika maeneo ya Goba, na
kituo kitakachojengwa na Kampuni ya DANGOTE Mkuranga. Aidha, TPDC
ilikwishatoa idhini kwa makampuni jumla 20 kujenga vituo vya CNG nchini.
Foleni
zinazoonekana kwa sasa katika kituo cha kujaza gesi asilia kwenye magari cha
Ubungo, zimetokana na hitilafu iliyotokea katika gari linalobeba gesi (CNG
tanker) kupeleka kituo cha Anric TAZARA, ambapo bomba lake la kupokelea CNG
limepasuka, na linafanyiwa matengenezo na kutarajiwa kuanza huduma mwishoni mwa
wiki ijayo.
Ni
matumaini yetu kwamba huduma katika kituo cha Anric TAZARA itarejea na
kupunguza adha inayoendelea kwa sasa, hata hivyo inatarajiwa kuwa ndani ya
miezi 24 vituo vya CNG vitaenea kwa wingi hapa nchini na kuondoa changamoto
zinazoonekana kwa sasa na kuwezesha wananchi wengi kunufaika na huduma hii.
Imetolewa
na;
Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
Jengo la PSSF Kambarage/ Ghorofa ya 8,
Mtaa wa Jakaya Kikwete
S.L.P 1191
DODOMA.
No comments:
Post a Comment