Sunday, 25 June 2023

DKT. TAX AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA WA ITALIA JIJINI ROMA

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Italia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Antonio Tajani ofisini kwake jijini Rome nchini Italia..

 

Akizungumza na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Tax ameelezea kuridhishwa na uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Italia na kuishukuru Serikali ya Italia kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuiletea maendeleo kupitia elimu, afya, kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa na uchumi wa buluu.

 

Mhe. Dkt. Tax ameihakikishia Italia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana nayo na kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Italia unakuwa na kufikia ngazi ya juu.



Dkt. Tax amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa majadiliano ya kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Italia ambao utatumika kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili kwa maslahi mapana ya pande zote.

 

“Nafahamu kuwa nchi zetu hazina mfumo wa majadiliano wa kisiasa na kidiplomasia licha ya kuwa na uhusiano mzuri wa siku nyingi, napendekeza tuanzishe mfumo wa majadiliano ya kisiasa na kidiplomasia kati ya nchi zetu, mfumo huu utatumika kama jukwaa la kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya nchi zetu kwa maslahi ya pande zote,” alisema Dkt. Tax.

Habari kamili na Ally Thabith

No comments:

Post a Comment