Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar Mussa Haji Mussa, amesema kubeza na kudhihaki mafanikio yaliyopatikana chini ya Muungano na Mapinduzi ya mwaka 1964 haviwezi kuwa tiketi ya kufikia malengo ya kisasa ya Chama Cha ACT-Wazalendo.
Kauli hiyo aliitoa Naibu Katibu Mkuu huyo, wakati akizungumza katika mahojiano maalum huko Afisi Kuu ya UVCCM Zanzibar Gymkhana, alisema mafaniko yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ni kielelezo tosha cha wananchi wa Zanzibar kuendelea kuamini,kupenda na kuunga mkono sera na siasa za CCM inayosimamia Serikali zote mbili nchini.
Alisema tabia za viongozi wa ACT-Wazalendo za kubeza na kudharau hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa chini ya tunu za Muungano na Mapinduzi ya mwaka 1964,haziwezi kuwatengenezea uaminifu wa kisiasa kwa wananchi kwani ni porojo zisizokuwa na dhamira ya kuleta maendeleo nchini.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Mussa, alisema baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakijisahau kwa kutumia majukwaa ya kisiasa kueleza uongo,upotoshaji na kuchochea ubaguzi dhidi ya taifa badala ya kushauri Serikali mambo yenye tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Chama cha ACT-Wazalendo wameishiwa na sera kwani badala ya kuibua hoja zenye mashiko na kuishauri Serikali mambo mema ya kuimarisha masuala mbalimbali katika nyanja za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kiutamaduni, wao wanabeza na kuzikashifu Serikali zilizowasomesha na Kuwapa madaraka waliyonayo hivi sasa.
Vyama vya upinzani nchini wanatakiwa wakae miaka zaidi ya 200 kutafakari kwa kina njia bora za kushindana na CCM katika medani za kisiasa katika dhana ya kidemokrasia kwani sisi kazi yetu ni kupanga,kufuatilia,kusimamia kisha kutenda kwa vitendo na hatimaye kutoa matokeo chanya yenye manufaa kwa wananchi wote”, alifafanua Mussa.
Mussa, alisema ACT-Wazalendo imeendelea kutumia vibaya haki ya mikutano ya hadhara kwa kukiuka dhamira ya ruhusa ya uwepo wa mikutano hiyo nchini iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, iliyokuwa na malengo ya kukuza demokrasia na ushindani wa kisasa na sio kauli za hoja za chuki dhidi ya Serikali.
Alisema hakuna mwananchi yeyote visiwani Zanzibar ambaye hakuguswa na dhulma,uonevu na ubaguzi wa utawala wa kigeni kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964, hivyo wanasiasa wanaojitokeza hivi sasa wakaunga mkono hadharani utawala huo watakuwa na ajenda za siri za kutaka kurejesha utawala huo jambo ambalo haliwezekani kwa zama za sasa.
Pamoja na hayo alieleza kwamba kupitia Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea kuwahudumia wananchi kwa uadilifu mkubwa sambamba na kuendelea kufungua milango ya uwekezaji na diplomasia zenye tija na maslahi kwa nchi.
Aidha, alisema UVCCM Zanzibar itaendelea kulinda,kutetea na kujenga hoja imara juu ya kupinga kauli na vitendo vyote visivyofaa katika michakato ya siasa za kidemokrasia vinavyofanywa na vyama vya upinzani kupitia majukwaa ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Pamoja na hayo Mussa, aliwapongeza Marais wote wawili ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 na kuibua miradi mikubwa ya maendeleo,inayoendelea kutoa fursa za ajira kwa vijana nchini.
No comments:
Post a Comment