Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tarehe 16 Juni, 2023 imesaini nyongeza ya kazi (Addendum) katika mikataba ya kupeleka nishati ya umeme vijijini ambapo sasa vijiji 4,071 vitapata nyongeza ya kilometa mbili za umeme wa msongo mdogo.
Tukio hilo la kusaini nyongeza ya kazi katika mikataba hiyo ya kupeleka umeme vijijini, liliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy pamoja na Wakandarasi 21 kutoka ndani na nje ya nchi huku pia likishuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene pamoja na Wajumbe wa Bodi hiyo katika ukumbi wa Ngome, Jijini, Dar es Salaam.
Baada ya hafla hiyo, Mhandisi Hassan Saidy alisema, hitaji la nyongeza ya kazi ya kupeleka umeme vijijini, lilianza kutolewa na makundi mengi ya watu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge pamoja na Wananchi wenyewe.
“Serikali ilisikia maombi yao, tunashukuru walitupa fedha na mwaka huu, tukaamua kuongeza kilometa mbili katika kila kijiji.”
“Mtakumbuka kuwa awali, kila kijiji kilipata kilometa moja (1) za umeme ambazo ni sawa na nguzo ishirini (20), sasa baada ya kusaini nyongeza hii, kupitia Mradi wa Kupeleka Nishati Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili (REA 3, II), hadi mwezi Desemba, 2023 vijiji hivyo 4,071 vitapata kilometa mbili zaidi.” Amekaririwa Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy amesema Watu wengi wameona umuhimu wa umeme katika kuleta maendeleo
pamoja na kubadilisha maisha yao kijamii na kiuchumi na kuongeza kuwa nyongeza hiyo ya kazi italeta mabadiliko makubwa kwa Watu.
“Jumla tumeongeza zaidi ya kilometa 8,000 kwa Mradi mzima wa REA 3, II kwa hiyo vijiji 4,072 vilivyopata umeme kwa kilometa moja (1), sasa kila kijiji kitapata kilometa mbili (2) zaidi.” Alisema Mhandisi Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA.
Habari picha na Ally Thabit
No comments:
Post a Comment