OTUBA YA WAZIRI KIVULI WA UTUMISHI WA UMMA, UTAWALA BORA NA MUUNGANO-ACT WAZALENDO NDG. PAVU ABDALLAH JUMA KUHUSU MPANGO WA BAJETI WA OFISI YA RAIS- MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.
Utangulizi.
Wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiendelea kupitia, kujadili na kuidhinisha bajeti mbalimbali za Serikali, jana Jumatano tarehe 19 April 2023, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Ndg. George Simbachawene (Mb) aliwasilisha Bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
Mpango huo una jumuisha mafungu saba (7) ambao yanagusa, Ofisi ya Rais-Ikulu (Fungu 20 na 30); Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Fungu 33); Utumishi na Utawala Bora (Fungu 32); Sekretarieti ya Ajira (Fungu 67); Tume ya Utumishi wa Umma (Fungu 94); na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (Fungu 04); Kutokana na umuhimu wake ni tumeona lazima liwepo jicho la kumulika, kufuatilia na kutoa mtazamo mbadala katika mpango huu.
ACT Wazalendo katika kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali, kupitia Waziri Kivuli wa Utumishi na Utawala bora imefuatilia na kuichambua hotuba hiyo kwa lengo la kuimulika ili kuona kwa kiasi gani imebeba matarajio ya wananchi katika kupata huduma na usimamizi wa rasilimali zao au vinginevyo. Kutokana na uchambuzi tulioufanya, tumekuja na maeneo saba (7) yenye changamoto na kuweka mtazamo mbadala wa ACT Wazalendo kuhusu hotuba hiyo ya Serikali, ambayo inaonyesha mambo ni yale yale.
Maeneo saba (7) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya Utumishi wa umma na Utawala bora kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
1. Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) iondoke Ikulu.
Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22 tuliofanya April 11, 2023 tulieleza maamuzi mabovu yaliyofanywa na Serikali mwaka 2016 kuhusu Wakala wa Ndege za Serikali.
Mosi, uamuzi wa kuipeleka TGFA kuwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kutoka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Pili, Wakala kuongezewa jukumu la kuratibu ununuzi wa ndege, kuzikodisha kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kusimamia mikataba ya ukodishwaji wa ndege hizo kwa niaba ya Serikali, mbali na jukumu lake la asili la kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa Kitaifa.
Tulieleza athari za uamuzi huo unathibitishwa na ripoti ya CAG, ambayo imeonyesha ATCL wanaendelea kupata hasara ya Shilingi bilioni 35 sambamba na Shirika hilo kuwa na mtaji hasi wa shilingi bilioni 158. Tuliweka wazi kuwa hasara inayopata ATCL kwa sehemu kubwa inatokana na mfumo wa umiliki wa ndege. Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Mfumo huu unaoleta hasara kwa taifa unatokana na uamuzi wa mwaka 2016.
Tunashangaa katika hotuba ya bajeti ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2023/24, tumeendelea kuona Wakala wa Ndege za Serikali inaratibu mpango wa ununuzi wa ndege na kuzikodisha kwa Kampuni ya Ndege ya Taifa (ATCL). Licha ya kushauriwa kutoendelea na uamuzi huu. ACT Wazalendo tunaona Serikali inataka kuendelea kuisababishia hasara ATCL kwa kung’ang’ania kutekeleza uamuzi mbovu wa huko nyuma.
Aidha, bado tunaona uamuzi uliofanywa kuhusu Wakala wa Ndege za Serikali kuwekwa chini Ofisi ya Rais Ikulu ni uamuzi usiofaa.
Kwasababu haukufanywa kwa ajili ya manufaa ya umma badala yake ulilenga kuzuia uwazi na uwajibikajika katika mikataba ya ununuzi wa ndege. Kitendo kilichopelekea kurudisha nyuma jitihada za kudhibiti ubadhirifu na ufisadi katika manunuzi ya ndege ambayo sasa yanalalamikiwa hata na Rais mwenyewe.
Hivyo basi, ACT Wazalendo tunarudia wito wetu wa kuitaka Serikali kuirejesha TGFA wizara inayohusika na Uchukuzi ili kudhibiti ubadhirifu na wizi kwa kuimarisha uwazi, kwakuwa bajeti ya wizara ina kaguliwa na ripoti yake inakuwa wazi.
Pili, tunaitaka Serikali imwagize CAG kufanya ukaguzi maalumu wa manunuzi ya Ndege tangu tulipoanza kununua ndege mwaka 2016.
Tatu, tunaitaka Serikali ifanye mapitio ya mikataba yote ya manunuzi ya ndege kwa lengo la kuiboresha kwenye mapungufu.
2. Kanuni mpya za mafao bado zinaumiza wazee wetu wastaafu.
Wizara ya Utumishi na Utawala bora pamoja na majukumu mengine ina wajibu wa kuhakikisha nidhamu, maadili na utendaji wa watumishi wa umma nchini. Suala la utendaji na nidhamu linahusiano wa karibu sana na ustawi, haki na maslahi ya watumishi hao.
Kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya watumishi wa umma wanaostaafu kupunjwa mafao yao tangu kuanza kutumika kwa kanuni mpya ya kikotoo cha mafao Julai 01, 2022.
Kanuni mpya ya ukokotoaji wa asilimia 33 na kikotoo cha 1/580 badala ya 1/540 kinapunguza malipo ya mkupuo (lumpsum) ya kiinua mgongo cha mtumishi anayestaafu kwa asilimia 50.5 ukilinganisha na kanuni za awali (kabla 2018).
Itakumbukwa kuwa ujio wa kanuni hizi, zilitokana na mvutano mkubwa mwaka 2018 baada ya Serikali kupeleka Bungeni muswada wa kanuni za mifuko ya hifadhi ya jamii iliyoambatana na kanuni mpya za kukokotoa mafao ya wastaafu. Kanuni hii (kikotoo) ilipingwa na wafanyakazi, wanaharakati na wanasiasa kila kona kwa hoja za wazi kabisa.
Kurejeshwa kwake mwaka jana (bila mwafaka wa pande mbili) ndio imeanza kuleta kelele, vilio na masikitiko kama sio kushusha hamasa na ari ya watumishi wengi nchini. Huku kikiwa na marekebisho madogo tu ya asilimia za mkupuo kutoka 25 iliyopendekezwa na Serikali yenyewe, hadi asilimia 33 lakini bado haiendi kuwasaidia wastaafu badala yake inaenda kuwaumiza.
Sisi, ACT Wazalendo tunaendelea kupinga utekelezaji wa kanuni hizi. Tunaamini hatupaswi kuwaadhibu wazee wetu kwa kukubali kanuni hizi kandamizi kuendelea kuwapunja mafao yao. Aidha, hatukubaliana na uamuzi wa Serikali kuwabebesha watumishi wanaostaafu mzigo wa gharama kwa makosa ya utendaji mbovu wa menejimeti za mifuko na madeni ya Serikali.
Hivyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kulipa madeni yote (Kiasi cha Shilingi trilioni 1.4) inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mkupuo mmoja ili kuiwezesha mifuko kujiendesha na kuhudumia wanachama wake kwa wakati.
Pia tunaitaka Serikali kurejesha kanuni za mwaka 2017 ambazo zinatoa mafao ya malipo ya mkupuo kwa 50%, kikokotoo kuwa ni 1/540, umri wa kuishi baada ya kustaafu ni miaka 15.5 na 50% inayobaki ya mafao ya mtumishi iwe pensheni ya kila mwezi.
3. Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Katika mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/24 wizara ya utumishi imeendelea na jukumu la kuratibu na kusimamia Miradi ya Maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Sisi, ACT Wazalendo katika kuangazia jukumu hili, tumekuwa tukielezea changamoto, hoja na mapendekezo ya namna bora ya kusimamia fedha za TASAF kufuatia na malalamiko mbalimbali tuliyoyapokea kutoka kwa wananchi.
Mosi, kuhusu utaratibu mpya wa Serikali maeneo mbalimbali nchini wa kuwafanyisha kazi ngumu wazee na watu wenye ulemavu kama kigezo cha kupatiwa fedha hizo za Tasaf. Wanufaika hao wanalazimishwa kufanya kazi za nguvu kama vile kuchimba mitaro, mabwawa, kufanya usafi kwenye shule au kufyatulishwa matofali badala ya kupatiwa fedha hizo kama ruzuku kutokana na kundi lao.
Pili, fedha hizo sasa hivi zinatolewa kwa ubaguzi au kutumika vibaya na viongozi wa Chama cha Mapinduzi ili kujinufaisha kisiasa kwa kuwatisha watu wenye vigezo vya kunufaika na TASAF kuwa hawatonufaika iwapo hawatajiunga na CCM au kuwaondoa kwenye mfumo ikiwa watakuwa Wapinzani wa CCM. Aidha, kutoeleweka kwa viwango wanavyopaswa kupewa wanufaika kwa mwezi au kipindi maalum inatoka bila utaratibu unaoeleweka hivyo kukwaza lengo la fedha hizo.
Katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imeiombea fedha cha Shilingi bilioni 218.9 kwa ajili ya walengwa TASAF nchini. Kutokana malalamiko ya wanufaika juu hoja hizi ni wazi wapo watu wanaopaswa kunufaika na fedha hizi watachwa nje ya mfumo huo.
ACT Wazalendo tunaendelea kumtaka Waziri mwenye wizara (Utumishi na utawala bora) husika kufuatilia kwa karibu, kujitokeza kutoa ufafanuzi na kuchukua hatua za kumaliza changamoto hizo Nchi nzima. Pia, CCM iache kulaghai watanzania fedha hizi ni za mkopo kutoka Benki ya Dunia na wahisani wengine, zinalipwa na watanzania wote bila ya kujali itikadi ya vyama vyao kwa kuwa watakatwa kupitia kodi mbalimbali, haikubaliki kuona watu wa chama au wasiokuwa wanachama wanabaguliwa.
Mwisho, tunaona ili kumaliza tatizo hili ni lazima Serikali iimarishe mfumo wa hifadhi ya jamii ili kutoa pensheni kwa wazee wote badala ya kutegemea fedha za Mkopo ambazo zinaweza kusitishwa mara moja.
4. Ubadhirifu wa fedha za Umma.
Sekta ya Utumishi wa umma ni muhimu sana kwenye mapambano dhidi ya ubadhirifu au kuchunga matumizi mazuri ya fedha za umma. Ingawa, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala bora ina wajibu huo. Bado tumeendelea kuona upotevu wa fedha, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma kwenye Ofisi, Idara na Halmashauri mbalimbali nchini.
Hoja ya ubadhirifu imekuwa ikirudiwa rudiwa kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Katika ripoti ya mwaka 2021/22 iliyotoka mwaka huu imeonyesha hali imendelea kuwa mbaya zaidi kuhusu upotevu wa fedha na ubadhirifu.
Mathalani hoja za ukaguzi zinazonyesha ubadhirifu kwa Wizara ya TAMISEMI peke yake zina thamani ya Shilingi bilioni 975. Vilievile, kuna matumizi mabaya ya fedha kwenye wizara ya Ujenzi na uchukuzi hoja za ukaguzi inafikia thamani ya Shilingi trilioni 4.6. Aidha, matumizi mabaya ya fedha za Mkopo wa UVIKO 19 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yameonekana kiasi cha shilingi bilioni 212.1 sawa na asilimia 17.06 ya fedha zote za mkopo zilitolewa ambazo ni shilingi Trilioni 1.24.
Katika hotuba ya Ofisi ya Rais Utumishi wa umma na utawala bora iliowasilishwa na Ndg.Waziri George Simbachawene haijaongelea kuhusu hatua ambazo zitachukuliwa juu ya watu waliotajwa kwenye ubadhilifu wa fedha za umma hii inaonyesha kwa namna gani serikali inashindwa kuwajibika na kuwachukulia hatua stahiki watu waliohusika katika ubadhilifu wa fedha hizo
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika katika ubadhilifu wa fedha hizi.
5. Kutomalizwa kwa madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa umma.
Katika uchambuzi tulioufanya mwaka jana (2022) wa bajeti na ripoti ya CAG tulionyesha kuwepo kwa malimbikizo ya muda mrefu ya mishahara, madeni na stahiki zilizotakiwa kulipwa kwa Watumishi wa Umma kiasi cha Shilingi bilioni 429.80 mwaka 2020/2021 kutoka shilingi bilioni 334.15 mwaka wa fedha 2019/2020. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 28%. Malimbikizo hayo yalitokana na watumishi kutolipwa kwa wakati, malimbikizo ya mishahara ya waajiriwa wapya, waliopandishwa madaraja, makato na posho za watumishi.
Katika taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2022/23 iliyotolewa na Waziri Bungeni ni imeonyesha kuwa Serikali imelipa jumla ya madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 119,098 yenye thamani ya shilingi bilioni 204.42. Hii ni hatua inayoleta matumaini kwa watumishi wa umma na wafanyakazi nchini. Ingawa, tumepatwa na mshangao kuona katika mwaka huu wa fedha hakuna mpango ulioanishwa wa kibajeti wa kumalizia malimbikizo yaliyobaki ambayo zaidi ya asilimia 50 ya madai (shilingi bilioni 225.5).
ACT Wazalendo tunarudia wito wetu kwa kuitaka Serikali kumaliza kwa mkupuo madai malimbikizo ya watumishi kupitia mfumo wa hatifungani maalum. Aidha, tunasisitiza Serikali kuyatambua madeni haya katika takwimu za deni la taifa na kuimarisha mfumo wa kulipa madai ya watumishi ambao utahakikisha kuwa madeni mapya hayatoozalishwa tena siku za usoni.
6. Mfumo wa ajira na upungufu mkubwa wa watumishi wa umma nchini.
Serikali kupitia wizara hii ndio inayoratibu masuala ya ajira ya watumishi wa umma kwa taasisi za Serikali kuu, idara na halmashauri. Mwenendo wa miaka mitano (5) hadi sasa unaonyesha kutoridhisha kiwango uwiano kati ya maombi ya vibali vya ajira kwa taasisi mbalimbali na ajira zinazoidhinishwa na kutolewa na Serikali.
Hii ina maana kuwa mahitaji ya watumishi katika taasisi, idara na Ofisi za umma na kasi ya ajira zinazoidhinishwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma haviwiani (haviendi sambamba). Mathalani mahitaji ya watumishi kwa Serikali Kuu na Idara kwa mujibu wa ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2021/22 inaonyesha kuwa kwa miaka mitatu yaani 2019/20, 2020/21 na 2021/22 mahitaji (vibali vilivyoombwa) vilikuwa 77,703, huku mpango wa kuajiri wa Serikali ulikuwa kuajiri watumishi 24,948. Lakini Serikali iliweza kutoa vibali 25, 602. Mwenendo wa jumla ya uajiri wa Serikali ukilinganishwa na mahitaji ni asilimia 35 tu. CAG anasema kuwa “Tatizo la upungufu wa Watumishi wa Umma bado ni kubwa na linasababishwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushindwa kutoa vibali kwa wakati. Hii inapelekea Taasisi za Umma kutofikia malengo ya kiutendaji.”
Aidha, hali ya upungufu wa wafanyakazi imezikumba zaidi Mamalaka za Serikali za Mitaa ambazo pia vibali vya kuajili vinategemea kupitia wizara hii. Hii inapelekea ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani kwenye sekta ya elimu na afya umeathirika kutokana na Watumishi waliopo kuzidiwa na majukumu.
ACT Wazalendo tunaitaka Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa vibali vya ajira kwa taasisi zinazohitaji wataalamu lakini pia kuhakikisha wataalamu wanaopatikana wana vigezo vya taaluma zao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
7. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanyiwe ukaguzi.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Sheria hii ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) Sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
TAKUKURU inaingia kwenye kundi la taasisi zilizowekwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kiasi cha kushindwa kumulikwa ufanisi wake kwa kuwianisha na matumizi inayofanya. TAKUKURU inatengewa fedha na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha TAKUKURU inapaswa kukaguliwa kila mwaka lakini tangu mwaka 2007 ilipoanzisha haijawahi kukaguliwa.
Kutokana na uzoefu wa utendaji, historia na tafiti mbalimbali licha ya kuwa ni chombo kilichoanzishwa ili kuimarisha uwajibikaji na kuchunga matumizi mazuri ya rasilimali yapo malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi kwa baadhi ya watumishi, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka taarifa za fedha zinazojitegemea za TAKUKURU sio kufichwa kwenye fungu la 20 la bajeti. Pia, tunaitaka Serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuifanya ukaguzi TAKUKURU kama sheria zinavyotaka na taarifa yake iwe wazi kwa umma.
Hitimisho
Mpango wa utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Menejimeti, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2023/24 unaonyesha bado mambo ni yale yale. Dhana ya utawala bora inazidi kudorora kufuatiwa na hoja za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma katika ofisi mbalimbali za Serikali kuu, idara na Halmashauri nchini. Aidha, kuendelea kuruhusu kutumika kwa kanuni mpya ya kikotoo cha mafao kwa watumishi wanaoenda kustaafu kunaporomosha ari na utendaji wa watumishi. Vilevile, suala la matumizi ya fedha za maendeleo ya jamii kutowekewa utaratibu mzuri kutaendelea kuchomwa fedha hizo bila kuleta matokeo tarajiwa.
Wizara ya Utumishi inapaswa kumulika uwajibikaji wa Serikali kwa kuimarisha vyombo vya kuisimamia serikali kama vile Ofisi ya Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Pia kuimarisha taasisi za usimamizi na ulinzi wa sheria kama vile, Usalama wa taifa, Tume ya Maadili ya Utumishi wa umma
No comments:
Post a Comment