Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema ameungana na timu ya Mkoa wa Iringa kushiriki doria ya kuwasaka wanyama aina ya Simba wanaosemekana wametoka katika maeneo yao ya asili na kuvamia vijiji vilivyoko jirani na Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuua mifugo kitu kinachosababisha taharuki katika maeneo wanayozurura.
Nilipata taarifa ya uvamizi wa wanyama hao katika vijiji vilivyoko mbali kabisa na hifadhi zaidi ya kilometa 25 lakini hadi sasa simba hao wameshaenda umbali wa zaidi ya kilometa 70 na wameshavuka barabara ya lami ya kutoka Morogoro, Iringa kwenda Mbeya na wako upande wa pili wa barabara wakiendelea kufanya uharibifu aliongeza Kamishna huyo.
“Baada ya uvamizi wa wanyama hao,timu ya askari 17 kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha na maafisa kutoka Kanda ya Kusini walifika kwa haraka kushirikiana na wenzetu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, TAWA na KDU kuwasaka Simba hao wasilete madhara zaidi” alisema Kamishna Makilema.
Aidha, Kamishna Mwakilema alisema kuwa kutokana na unyeti wa jambo hili tulifanya jitihada za kupata Helikopta na jana wasaidizi wangu wameruka nayo ila kutokana na hali halisi ya milima na makorongo marefu hawakuweza kuwaona. Pia nimeongea na mtu wa AWF pale Manyara Ranch ili kuweza kupata mbwa wa kunusa watusaidie kutambua harufu za Simba hao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy alisema kuwa wilaya imeingiwa na taharuki kubwa baada ya kupata taarifa ya uwepo wa Simba katika Kata ya Magoma na kuua ng’ombe. Kwa haraka niliwasiliana na wenzetu wa TANAPA na TAWA kuja kuwaondoa Simba hao.
Hata hivyo, Simba hao waliendelea kusonga mbele wakiua mifugo na hatimae kufika eneo la Kiponzelya karibia na mji wa Iringa. Hadi kufika tarehe 24.06.2023 Simba hao wameshaua ng’ombe 25, na kujeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu, pia wameua mbuzi 5, kondoo 5, nguruwe 3 na kuku1 aliongeza mkuu wa wilaya huyo.
Mkazi wa kijiji cha Tanangozi Grayson Laurent Mtende alisema, “baada ya kupata taarifa za Simba kijijini kwetu tuliogopa kwa sababu Simba hawazoeleki na ni mnyama anayeogopwa hivyo tumesitisha kufanya kazi zetu mashambani kwa muda mpaka pale mamlaka zinazohusika na uhifadhi zitakapotuambia hali ni shwari”.
Simba hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 5 bado hawajaonekana na jitihada za kuwasaka zinaendele kwa kutumia magari, helikopta na jitihada za kupata mbwa wa kunusa zinaonyesha kuzaa matunda. Pia wananchi wanaendelea kuelimishwa njia salama za kujilinda na wanyama kwa kutokuwaruhusu watoto na watu wazima kwenda vichakani kuokota kuni, na wanapotoka nje nyakati za usiku watoke na tochi.
No comments:
Post a Comment