Na Mwandishi wetu
1/10/2019 Madaktari nchini wameshauriwa kuwatuma watoto wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mapema iwezekanavyo mara baada ya kuwagundua kuwa na matatizo hayo ili waweze kupata matibabu kwa wakati.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kwa watoto (JKCI) Naiz Majani wakati akizungumzia kuhusu kambi ya matibabu ya magonjwa ya moyo ya ya kuzaliwa nayo kwa watoto ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo iliyomalizika mwishoni mwa wiki katika Taasisi hiyo.
Dkt. Naiz ambaye pia ni msimamizi wa kambi za matibabu ya moyo zinazofanyika katika Taasisi hiyo alizitaja dalili za mtoto mwenye magonjwa ya moyo kuwa ni pamoja na kutokwa na jasho kwa wingi wakati wa kunyonya, kutoongezeka uzito, kupata nimonia, kikohozi cha mara kwa mara , kushindwa kucheza , kuvimba miguu na kubadilika rangi kwenye midomo na kucha kuwa rangi ya bluu.
“Ninawaomba madaktari wanapoona dalili kama hizi kwa mtoto wawalete katika Taasisi yetu kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi kwani kuna baadhi ya matatizo ya moyo ya kuzalliwa nayo mtoto hatakiwi kuzidi umri wa miezi sita hadi mwaka mmoja bila ya kupata matibabu. Mtoto mwenye matatizo hayo akichelewa kupata matibabu akiwa na umri huo hawezi kufanyiwa upasuaji tena”, alisisitiza Dkt. Naiz.
“Katika kambi ya matibabu ya pamoja tuliyoyafanya na wenzetu wa Shirika la Mending Kids International lenye wataalamu wa afya kutoka nchini Italia na Marekani watoto wanne walishindwa kufanyiwa upasuaji kutokana na umri wao kuwa mkubwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu hivyo wataendelea na matibabu ya kawaida”, alisema Dkt. Naiz.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Dkt. Naiz alisema watoto 40 walifanyiwa upasuaji kati ya hao watoto waliofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua 17 na upasuaji wa bila kufungua kifua 23 ambapo hali zao zinaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kurudi nyumbani.
Dkt. Naiz alisema, “Kambi hii imeenda vizuri, kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama, wakati huduma za upasuaji zinaendelea kwa watoto walijitokeza wasamaria wema wawili na kuchangia matibabu ya watoto wawili ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwagharamia matibabu. Watoto hao wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri”, alisema Dkt. Naiz.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao walipata wafadhili wa kulipiwa gharama za matibabu walishukuru kwa huduma ya matibabu ambayo watoto wameipata na kuwaomba wadau wengine wajitokeze kuchangia gharama za matibabu ya moyo kwa watoto.
“Namshukuru mfadhili wa mtoto wangu ambaye amelipa gharama za matibabu ya mtoto ambaye amefanyiwa upasuaji na hali yake inaendelea vizuri. Mara kwa mara amekuwa akinipigia simu na jana amekuja kumuangalia mtoto kujuwa maendeleo yake”, alisema Eva Jacob
No comments:
Post a Comment