|
|
MACHI
– MEI, 2024
Kielelezo 1: Mwelekeo wa mvua za Machi hadi
Mei, 2024.
Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Masika; Machi -
Mei 2024 Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na
mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha Machi – Mei, 2024,
ushauri kwa wadau wa sekta na mamlaka mbalimbali kama vile Kilimo na Usalama
wa Chakula, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Uchukuzi, Mamlaka za
miji, Nishati, Maji na Madini, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Baadhi ya
mambo muhimu katika taarifa hii ni: -
i. Mvua
za Wastani hadi Juu ya Wastani kwa msimu wa Masika, 2024 zinatarajiwa katika
maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
ii. Ongezeko la mvua linatarajiwa katika
kipindi cha mwezi Machi, 2024.
iii. Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza
wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024 katika maeneo mengi na zinatarajiwa
kuisha katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024 katika maeneo mengi. Athari zinazotarajiwa:
i. Vipindi
vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri
ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
ii. Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa
kuongezeka.
iii. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na
uchafuzi wa maji. |
1.
MWENENDO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA,
2023 HADI APRILI, 2024) NA MWELEKEO
WA MVUA ZA MASIKA (MACHI – MEI), 2024
1.1
Mwenendo wa
mvua za Msimu (Novemba, 2023 hadi Aprili, 2024)
Mvua za Msimu zilizoanza
mwezi Novemba, 2023 zimenyesha kwa kiwango cha Juu ya Wastani katika mikoa ya
Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Katavi, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na
kusini mwa mkoa wa Morogoro na Wastani katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe na
Njombe katika kipindi cha Novemba, 2023 hadi Januari, 2024. Mvua hizi zilianza
mapema wiki ya kwanza na ya pili mwezi Novemba, 2023 na zilitawaliwa na vipindi
vya mvua nyingi zilizochangiwa na uwepo wa El Niño. Katika kipindi kilichosalia
cha msimu (Februari hadi Aprili, 2024) mvua zinatarajiwa kuendelea kama
ilivyotabiriwa mwezi Oktoba, 2023, ambapo kwa ujumla mvua zilitabiriwa kuwa za Wastani
hadi Juu ya Wastani.
1.2
Mwelekeo wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2024
Msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo
ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro),
pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha
visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba),
ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na
Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa
inayotarajiwa katika kipindi cha Masika (kama inavyoelezwa katika kipengele Na.
2 cha taarifa hii), kwa ujumla mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa
katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Ongezeko la
mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2024 katika maeneo hayo. Maelezo ya kina juu ya
mwelekeo wa mvua hizo za msimu ni kama ifuatavyo:
i. Kanda
ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara)
pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo):
Mvua za Masika zinatarajiwa kuwa za Wastani
hadi Juu ya Wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha
zinatarajiwa kuungana na mvua za Masika 2024. Mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu
na ya nne ya mwezi Mei, 2024.
ii. Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (kaskazini mwa mkoa wa
Morogoro, mkoa wa Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam, Tanga
pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika
maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini.
Mvua hizo
zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024 na kuisha wiki
ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024.
iii. Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Arusha,
Manyara na Kilimanjaro):
Mvua katika maeneo
haya zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Juu ya Wastani na zinatarajiwa kuanza mapema
wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya pili
na ya tatu ya mwezi Mei, 2024.
|
||
Kielelezo 2: Kushoto: Mwelekeo wa mvua za
Masika (Machi –Mei), 2024 na Kulia: Wastani wa muda mrefu (miaka 30) wa mvua
za Masika (1991-2020). |
|
|
Angalizo 1: Izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza
katika Msimu wa Masika, 2024.
Angalizo 2: Mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi
mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia
mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo
utazingatiwa katika
uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa hii
wanashauriwa kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na
tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
2. MIFUMO YA HALI YA HEWA
Joto la bahari la juu
ya wastani linatarajiwa katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya
Afrika Mashariki) ikilinganishwa na upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi.
Vilevile, joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la
kusini mwa kisiwa cha Madagaska. Hali hii kwa pamoja inatarajiwa kuimarisha
mifumo isababishayo mvua nchini kwa kuimarisha kasi na nguvu ya msukumo wa
unyevu nyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya pwani ya kaskazini na
nyanda za juu kaskazini-mashariki. Katika eneo la mashariki mwa bahari ya
Atlantiki (pwani ya Angola), joto la bahari la chini kidogo ya wastani
linatarajiwa. Hali hii inatarajiwa kuimarisha msukumo wa unyevu nyevu kutoka
misitu ya Kongo kuelekea nchini hususan katika maeneo yanayozunguka ziwa
Viktoria, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Hata hivyo, hali ya El-Niño inayoendelea katika Bahari ya Pasifiki inatarajiwa
kupungua nguvu hususan tunapoelekea mwishoni mwa msimu wa mvua wa MAM, 2024.
3.
ATHARI NA USHAURI
Athari za kisekta na
ushauri uliotolewa hapa chini umeandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
kwa kushirikiana na wataalam wa sekta husika katika mkutano wa wadau wa hali ya
hewa uliofanyika tarehe 19 Februari, 2024. Wadau wa sekta mbalimbali za
kiuchumi na kijamii wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa
kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.
a)
Kilimo na Usalama wa
Chakula
Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko
vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
Magonjwa kama vile ukungu (Fungus) yanatajariwa kuongezeka na kuathiri mazao
kama nyanya, ufuta, maharage na mazao jamii ya mizizi. Hata hivyo, shughuli za
kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi.
Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na
kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia
maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba, na kuchagua mbegu na
mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa Masika. Pia, wanashauriwa kuimarisha
miundombinu ya kilimo hususan maeneo ya mabondeni pamoja na kudhibiti visumbufu
vya mimea ili kupunguza athari
zinazoweza kujitokeza. Aidha, wauzaji na wasambazaji wa
pembejeo za kilimo wanashauriwa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati.
b)
Mifugo na Uvuvi
Wafugaji na wavuvi
wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho na chakula cha samaki. Hata
hivyo, mlipuko wa magonjwa ya mifugo kama vile ugonjwa wa homa ya bonde la ufa
na kuzaliana kwa wadudu wanaosambaza magojwa vinaweza kujitokeza. Vilevile, matukio ya kuongezeka kwa magonjwa
ya mwani baharini na kupungua kwa uzalishaji wa mwani kutokana na kupungua kwa
kiwango cha chumvi ya maji ya bahari vinatarajiwa.
Wafugaji wanashauriwa kutumia
mbinu bora za ufugaji ili kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi
ya baadae. Jamii inashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi bora ya maji na
malisho. Wakulima wa mwani wanashauriwa kulima mwani kwenye maji ya kina kirefu
ili kuondokana na athari za maji ya mvua yanayokuwa yanaingia baharini. Vilevile,
wafugaji na wavuvi wanashauriwa kufuatilia mirejeo ya tabiri za hali ya hewa na
ushauri kutoka kwa maafisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na
kuongeza tija katika msimu huu wa mvua.
c)
Utalii na Wanyamapori
Hali ya malisho na maji kwa ajili ya wanyamapori katika mbuga
na hifadhi inatarajiwa kuwa nzuri. Hata hivyo, mvua za wastani hadi juu ya
wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi zinaweza kusababisha kutuama na
kusambaa kwa maji na kupelekea kuhama kwa wanyamapori. Hali hii inaweza
kupelekea magonjwa ya wanyamapori kusambaa kwa wanyama wanaofugwa na binadamu
kutokana na wanyamapori kuingia katika makazi ya jamii zinazozunguka hifadhi na
mbuga. Pia, hali hii inaweza kusababisha hatari kwa binadamu na wanyama
wanaofugwa kutokana na kushambuliwa na wanyamapori.
Mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu mbalimbali
katika hifadhi za wanyamapori na kujenga uelewa kwa jamii ili kupunguza athari
zinazoweza kujitokeza. Hivyo basi, jamii inashauriwa kutoa taarifa kwa mamlaka
husika endapo wanyamapori wataingia katika makazi ya watu.
d)
Usafiri na Usafirishaji
Kutokana na mvua zinazotarajiwa, sekta ya usafiri na
usafirishaji inatarajiwa kuathirika na kupelekea uharibifu wa miundombinu ya
barabara na reli, ongezeko la ajali barabarani katika usafiri wa nchi kavu,
kuchelewa au kusitishwa kwa safari za nchi kavu, ndege, majini,
mawasiliano hafifu angani na kwenye maji na kupelekea
kuongezeka kwa gharama za uendeshaji katika usafiri wa anga, nchi kavu na
majini. Mamlaka husika na wadau wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika
utekelezaji wa matengenezo na ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na
ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili
kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
e)
Nishati, Maji na Madini
Mvua zinazotarajiwa zitachangia kuongezeka kwa kina cha maji
katika mito, maziwa na mabwawa hivyo matumizi sahihi ya maji majumbani na
uzalishaji wa umeme ni muhimu kupewa kipaumbele. Hata hivyo, kupungua kwa ubora
wa maji, kuongezeka kwa kifusi cha mchanga maji na uharibifu wa kingo za mito
na mtandao wa usambazaji maji pia unatarajiwa.
Sekta ya Madini hususan shughuli za uchimbaji mdogo wa
madini, huenda zikaathirika, hivyo tahadhari za kiusalama ni muhimu kuchukuliwa
ili kukabiliana na maporomoko ya ardhi na miamba. Mvua zinazotarajiwa huenda
zikaathiri mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme na
kupelekea kukosekana kwa umeme. Hivyo, mamlaka husika na wadau zinashauriwa
kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali maji na mgawanyo wake kwa maeneo
mbalimbali kama vile shughuli za uchakataji madini, uzalishaji umeme, matumizi
ya viwandani na majumbani.
f)
Mamlaka za Miji na
Wilaya
Vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha kutuama kwa maji
na mafuriko. Hali hii inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na upotevu
wa maisha na mali. Mamlaka za Miji na Kamati za Maafa zinashauriwa kuchukua
hatua stahiki ili kukabiliana na athari zinazohusiana na mafuriko ikiwa ni
pamoja na shughuli za utafutaji, uokoaji na msaada wa kitabibu.
g)
Sekta ya Afya
Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa
miundombinu ya maji unaoweza kusababishwa na maji ya mvua kutuama na
kutiririka. Mamlaka za Afya na jamii
zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki ili kupunguza athari za kiafya
zinazotarajiwa kwa kuharibu mazalia ya mbu, kutibu maji kabla ya kuyatumia,
kunywa maji safi na salama pamoja na kuhakikisha uwepo wa dawa na vifaa tiba
vya kutosha katika vituo vya Afya.
h)
Sekta Binafsi
Sekta binafsi inatarajiwa kunufaika na mvua zinazotarajiwa
katika msimu huu wa Masika hususan katika shughuli za kilimo, uzalishaji
viwandani, n.k. Hata hivyo, wingi wa mvua unaweza kupelekea athari katika shughuli
za ujenzi wa miundombinu, uhifadhi na usafirishaji wa mazao tete na bidhaa.
Sekta binafsi zinashauriwa kushirikiana na wataalam
mbalimbali ikiwemo wataalam wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari
zinazoweza kujitokeza. Taasisi mbalimbali zikiwemo Benki na Bima zinashauriwa
kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau ili kujenga ustahamilivu katika
biashara.
i)
Menejimenti za Maafa
j)
Vyombo vya Habari
Vyombo vya Habari vinashauriwa
kupata, kufuatilia na kusambaza taarifa za utabiri na tahadhari, pindi tu
zinapotoka ili jamii iweze kuzipata kwa wakati. Vilevile, vinashauriwa kutafuta
ushauri wa kitaalamu kutoka katika sekta husika wakati wa kuandaa, kutayarisha
na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji. Pia, inapendekezwa kutumia
lugha nyepesi wakati wa kuhabarisha jamii.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri
watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,
wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji, afya,
shughuli za ujenzi (Makandarasi), uchimbaji madini, upakuaji na ushushaji
mizigo Bandarini kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam
katika sekta husika.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya
mwelekeo wa mvua na hali ya hewa kwa ujumla nchini kadri
inavyohitajika. Aidha, wadau
wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za mwelekeo na
utabiri wa hali ya hewa ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Imetolewa: Tarehe 22 Februari, 2024.
Na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:
Bahari Picha na Ally Thabiti
No comments:
Post a Comment