Jopo la kupitia maamuzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) linaloundwa na wajumbe wa nne (4) limezinduliwa rasmi leo Juni 2, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jopo hilo, Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu J. Suluo amesema kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA kupitia kikao chake maalum kilichofanyika Dodoma tarehe 7 Februari, 2023, iliwateua wajumbe wa nne (4) wa Jopo hilo ambao ni Bw. Mohamed R. A. Mpinga, Mhandisi John Ngaraguza, Wakili Theresia Michael Clemence, pamoja na Wakili Asma Selemani Mohamed.
Aidha, CPA Suluo amesema, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA Prof. Ahmed Mohamed Ame, alimteua Bw. Mohamed R. A. Mpinga kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Mapitio. Bw. Mpinga ni Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mstaafu.
Vilevile amesema, Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA kwa mujibu wa kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 inapaswa kuunda Jopo la kupitia maamuzi ya Mamlaka linalohusisha watu wawili (2) wenye uzoefu wa masuala ya Sheria na waliofanya kazi kwa angalau miaka kumi (10) pamoja na watu wawili (2) wenye uzoefu wa angalau miaka kumi (10) kwenye masuala ya Uchumi, Fedha, Uhandisi au Usimamizi wa Usafiri.
CPA Suluo ameongeza kuwa, maamuzi yatakayoshughulikiwa na jopo hilo ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kwa mtu yeyote ambaye hatoridhishwa na maamuzi ya Mamlaka anaweza ndani ya siku 14 tangu kutolewa maamuzi hayo, kuomba maamuzi hayo yapitiwe,
CPA Suluo amesema, “Tunaishukuru Bodi yetu kwa kuwateua na tunaamini mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi wa hali ya juu kwa kuzingatia kuwa Mamlaka inatoa maamuzi na endapo mtoa huduma hajaridhishwa na maamuzi hayo basi atawasilisha kwenu ili kupitia upya maamuzi tuliyoyafanya na hatimaye jopo litatoa mapendekezo yake kwa Bodi ili iweze kufanya maamuzi kwa jambo husika. Endapo maamuzi hayo hayataridhiwa na mleta maombi, anaweza kukata rufaa kwa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal-FCT) kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413,” ameeleza CPA Suluo.
Baada ya uzinduzi huo, wajumbe hao wamepewa semina ya Sheria, Kanuni, wajibu na majukumu ya Mamlaka ili ziwaongezee uelewa wakati wa kutekeleza majukumu yao.
habari kamili na Ally Thabit
No comments:
Post a Comment