Friday, 28 July 2023

TANESCO YAZINDUA MPANGO WA JINSIA (GENDER WORK PROGRAM) WA MIAKA MINNE

 Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZA).

 

Progamu hii imezinduliwa na Mgeni Rasmi na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ukiwa na lengo la kutatua changamoto wanazokutana nazo wafanyakazi wanawake katika maeneo yao ya kazi na kuongeza uwiano wa utendaji kazi baina ya wanawake na wanaume kati ya mwaka 2023 hadi 2026.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mhe. Byabato alisema TANESCO imejizatiti kwa kiasi kikubwa kwenye usawa wa kijinsia na kuitaka menejimenti ya Shirika hilo kuhakikisha inaanzisha kitengo maalumu cha jinsia ili kuwepo na uwanja mpana wa kujadili masuala ya kijinsia.

 

“Naiagiza menejimenti ya TANESCO kupitia mradi wa TAZA kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele sawa na wanaume na kuongeza fursa zaidi kwa wanafunzi wa vyuo ambao wanajiandaa kuajiriwa kwenye ajira rasmi”.

 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande alisema, “Sisi kama TANESCO swala la kijinsia lipo juu kabisa katika agenda zetu. Wakati tunaanda mkakati wa Shirika, tuliainisha vipaumbele saba na katika kipaumbele cha kwanza kilikuwa ni kipaumbele cha watu na tuliweka masuala ya usawa wa kijinsia na hususani tuliweka mikakati ya kuhakikisha tunaongeza  viongozi wanawake katika Shirika letu”.

 

Ameyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na sera ya Shirika kutoa kipaumbele kwenye masuala ya jinsia, upatikanaji wa taarifa sahihi za masuala ya jinsia kwenye taasisi na kuwepo kwa nafasi za mafunzo ya ukuzaji taaluma kwa wafanyakazi wanawake hasa wanaofanya kazi za kiufundi ili kuwajengea uwezo kupitia mpango wa mafunzo kazini.

 

Akifunga uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Fedha wa TANESCO, CPA Renata Ndege alisema nafasi za wanawake kwenye Shirika zipo nyingi isipokuwa wengi wao wanakosa ujasiri wa kupambanania nafasi husika na wanafanyakazi wanaume.

 

Aidha, amepongeza hatua ya uanzishwaji wa kitengo maalum cha kushughulikia mambo ya jinsia kwani kitendo hiki kitaongeza kasi kwa wafanyakazi wanawake kuwepo kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

 

Mradi wa upanuzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka kituo cha kupokea, kupoza na kusairisha umeme cha Tagamenda Iringa nchini Tanzania kwenda Zambia (TAZA) na nchi nyingine zilizopo Kusini mwa Tanzania kupitia Kisada Iringa, Iganjo Mbeya na Nkangamo Tunduma Songwe unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia mkopo wa Jumuiya ya  Maendeleo ya Kimataifa (IDA) ya Benki ya Dunia, mkopo wa Mfuko wa Maendeleo wa Ufaransa (AfD), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


habari kamili na Ally Thabith

No comments:

Post a Comment