Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) amewapongeza madereva 999 waliofanya mtihani na kuthibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na amewasihi ambao hawakufaulu kutokata tamaa bali wajikumbushe tena yale waliyojifunza na warudi kufanya mitihani ili wathibitishwe.
Mhe. Mwakibete amesema hayo kwenye ufunguzi wa hafla ya uzinduzi wa Mtaala na Utoaji wa Vyeti kwa Madereva wa Vyombo vya Moto Vinavyotoa Huduma Kibiashara Waliothibitishwa na LATRA iliyofanyika Julai 01, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Arnaoutoglou, Dar es Salaam.
“Ninaamini hata wale ambao hawakufaulu, wamejikumbusha mambo kadhaa na niwasihi wasikate tamaa bali wajikumbushe tena yale waliyojifunza na warudi kufanya mitihani hii ili wathibitishwe na tuje kuwapatia vyeti siku chache zijazo,” ameeleza Mhe. Mwakibete.
Vilevile amesema kuwa, juhudi za LATRA za kuthibitisha madereva zitaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri ardhini nchini kwa kubadili tabia za madereva wakiwa barabarani na kutakuwa na tofauti ya dereva aliyethibitishwa na LATRA na yule ambaye hakuthibitishwa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji.
Aidha, Mhe. Mwakibete amezungumzia faida za kuwathibitisha madereva, “Serikali inaamini kuwa hadhi ya madereva itaongezeka, wataheshimika zaidi na maslahi yao yataboreshwa na zaidi, taaluma hii ya udereva itarasimishwa na kuwaongezea madereva thamani kwenye masoko ya ajira ya ndani na nje ya nchi, hususan kwenye nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),” amefafanua Mhe. Mwakibete.
Naye Mhe. Jumanne Sagini (Mb), Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani amesema zaidi ya asilimia 76 ya ajali zinazotokea barabarani zinasababishwa na makosa ya kibinadamu na hivyo amewaasa madereva hao kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani ili kupunguza na kuondoa kabisa ajali hizo.
Vilevile, ameipongeza LATRA kwa kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo Jeshi la Polisi, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na VETA kwa kuandaa kwa pamoja maswali yenye nia njema ya kufahamu uelewa wa madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma kibiashara.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo amesema Kanuni ya 22(i) ya Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria), 2020 inaainisha moja ya masharti ya leseni zinazotolewa na LATRA ambapo inawataka wenye vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara, kuhakikisha kila dereva anayeendesha vyombo hivyo wanakuwa na Cheti cha Uthibitisho kinachotolewa na Mamlaka baada ya kufanya mtihani na kufaulu,
Vilevile amesema kuwa, kabla ya kuanza kutahini madereva, Mamlaka kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ilipitia maswali ya mtihani yanayotumika kwenye vyuo vinavyozalisha madereva nchini kulingana na mitaala inayotumika na kuyaweka katika mfumo wa Kutahini Madereva (DTS).
Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, maswali hayo yanawapima madereva kuhusu uelewa wao kwenye maeneo ya alama na miongozo mbalimbali inayowasaidia kuendesha vyombo vya moto kwa usalama, “Baada ya maswali kupitishwa na kuwekwa kwenye mfumo, tarehe 1 Juni, 2022 Mamlaka ilianza rasmi kutumia mfumo wa DTS kutahini madereva ambapo hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2023 jumla ya madereva 1,744 walikuwa wamefanya mtihani na madereva 999 walifaulu.”
“Kwa kuwa tunawajali madereva wetu na tunataka wafaulu kwa wingi, LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, tumeandaa video mbalimbali zinazoelimisha kuhusu masuala ya msingi ya kuzingatia ukiwa barabarani ikiwemo suala la alama. Video hizi zinapatikana katika Online TV ya Mamlaka inayopatikana kwa jina la latraTV kwenye mtandao wa YouTube, hivyo ninawasihi wakatazame ili kujielimisha zaidi kabla ya kuja kufanya mtihani,” amesema CPA Suluo
Habari picha na Ally Thabit
No comments:
Post a Comment