Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Beno Malisa amewaasa wasafirishaji wa abiria na mizigo Mkoani Mbeya watimize wajibu wao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za usafirishaji.
Mhe. Malisa amesema hayo Juni 26, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera katika mkutano wa wadau wa usafirishaji abiria na mizigo ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kujadili changamoto za usafirishaji.
“Kwa kuwa jukumu hili la kujadili na kutoa maoni ya uboreshaji huduma za usafirishaji lipo kisheria, basi nawasihi kila mmoja wetu kwa kuzingatia umuhimu wa kazi hii atimize wajibu wake kwa umahiri wa hali ya juu,” ameeleza Mhe. Malisa
Pia, ameipongeza LATRA kwa kuandaa mkutano huo na kuwa hatua hiyo inaonesha LATRA inavyowajali watoa huduma wa usafiri ardhini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo amesema sekta ya usafirishaji ni moja kati ya sekta muhimu nchini kwani kila mmoja anahitaji huduma hii ya usafiri ili kutimiza wajibu wake wa kila siku.
“Huduma hii ya usafiri ni ya umuhimu katika jamii yoyote na ina mchango mkubwa katika uchumi na ustawi wa jamii yoyote ile duniani hata kufika hapa wote tumekuja kwa usafiri wa aina mbalimbali,” ameeleza CPA Suluo.
Vile vile amewapogeza wadau wa usafirishaji wa abiria na mizigo mkoani humo kwa kuacha shughuli zao muhimu na kuhudhuria mkutano huo.
Naye Mwenyekiti wa Wasafirishaji mkoa wa Mbeya Bw. Elias Mwanginde amesema kuwa, wasafirishaji wa mkoa huo wameona nuru kupitia uongozi wa sasa wa LATRA, hivyo watashirikiana kwa ukaribu ili kutekeleza mambo waliyokubaliana katika mkutano huo.
“Tunaona LATRA sasa ina uongozi imara na kutakuwa na mabadiliko, tunashukuru kwa elimu na majibu mazuri tuliyopata kwa maswali tuliyowauliza. Kupitia mkutano huu tumejulishwa kuwa Kituo cha LATRA cha Kutahini Madereva kiko tayari, pia leo hii tumetangaziwa fursa na wenzetu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kuwa wako tayari kuwapiga msasa madereva wetu ili kuwakumbusha mambo ya kuzingatia wakatapoenda kufanya mtihani wa kuthibitishwa,” amesema Bw. Mwanginde
Kwa upande wake, Bw. Muntazir Kassamia, msafirishaji wa mizigo amesema kuwa, mkutano huo umejenga uhusiano mzuri baina ya wasafirishaji na Serikali kwa kuwa baadhi ya changamoto zimeweza kutatuliwa kwa wakati na zingine zinafanyiwa kazi.
“Leo tumefaririjika sana kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA katika mkoa wetu wa Mbeya na tulikuwa na changamoto zetu ndogo ndogo na tunashukuru kwa uweledi na busara zake kuna mambo mengine ameyapatia ufumbuzi papo kwa papo, baada ya kupewa elimu na uamuzi alioufanya kwa kweli ametengeneza uhusiano mzuri sana baina ya LATRA na wasafirishaji mkoani hapa,” amesisitiza Bw. Kassamia.
Naye Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Mbeya SP Hussein Gawile amesema, “Kikao cha leo kimeleta hamasa kubwa sana kwa wamiliki maana leo wamepata ufumbuzi wa changamoto zao na mengi ambayo yamezungumzwa ni yale yatakayo leta athari chanya kwenye tasnia hii ya usafirishaji nchini.”
LATRA imekua na utaratibu wa kuandaa mikutano mbalimbali ya wadau wa usafirishaji nchini kwa lengo la kutoa elimu pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya Mamlaka na wadau wa usafirishaji ili kuleta maendeleo katika sekta ya usafiri ardhini nchini.
Habari kamili na Ally Thabit
No comments:
Post a Comment