Wednesday, 29 May 2019

MADAKTARI BINGWA WA MIFUPA MOI WAPEWA MBINU MPYA ZA UPASUAJI

 Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la madaktari bingwa wa mifupa linalofanyika Tanzania (MOI) Kuanzia tarehe 26 -30 May 2019 katika ukumbi mpya wa mikutano MOI. (PICHA ALLY THABITI)
 Madaktari wa Mifupa kutoka mataifa mbalimbali wakifuatilia mada katika kongamano la kimataifa linalofanyika MOI
 Madaktari wa Mifupa kutoka mataifa mbalimbali wakifuatilia mada katika kongamano la kimataifa linalofanyika MOI
 Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) katika kongamano la kimataifa la madaktari bingwa wa mifupa linaloendelea Kuanzia tarehe 26 -30 May 2019 ukumbi mpya wa mikutano MOI

NA KHAMISI MUSSA


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI Dkt. Respicious Boniface leo amefungua kongamano la kimataifa la madaktari wa Mifupa linalofanyika kwa siku tano hapa Tanzania ambapo madaktari zaidi ya 150 kutoka mataifa ya Afrika na sehemu mbalimbali duniani wanashiriki.


Dkt. Boniface amesema Kongamano hilo limekua likifanyika hapa nchini kila mwaka kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu mpya za matibabu ya mifupa madaktari hapa nchini na nchi nyingine barani Afrika kutokana na MOI kuwa kituo cha mafunzo na huduma bora za mifupa inazotozitoa.


“Madaktari bingwa wetu hapa nchini wamekua wakinufaika sana na kongamano hili, wamekua wakipewa mbinu mpya na za kisasa za matibabu na upasuaji wa mifupa jambo ambalo limepelekea MOI kuweza kumaliza rufaa za nje ya nchi kwa wagonjwa wa mifupa ambapo kwa sasa huduma karibia zote zinapatikana hapa nchini” Alisema Dkt Boniface.


Mratibu wa Kongamano hilo Dkt. Joseph Mwanga amesema mafunzo yatatolewa kwa njia ya nadharia, vitendo katika chumba cha maabara kwa kutumia mifupa bandia na kwenda kwenye chumba maalum cha kujifunzia kwa kutumia miili ya binadamu (Cadavers).


“Kongamano hili limekua na manufaa makubwa sana kwetu, tumekuwa tukipata mbinu mpya kila mwaka kutoka kwa wenzetu wa Marekani jambo ambalo limefanya huduma za mifupa hapa nchini ziendelee kuwa bora ukilinganisha na mataifa mengine barani Afrika” Alisema Dkt Mwanga.


Kwa upande wake Profesa Michael Terry ambaye ni mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Calfonia cha San Francisco amesema ushirikiano kati ya Taasisi yake na MOI umejikita katika mafunzo ya namna ya kuwahudumia majeruhi wa ajali kwa lengo la kuwapa huduma bora na za kisasa kwa wakati.


Kongamano hilo limeratibiwa na Taasisi ya MOI kwa kushirikiana na Taasisi za IGOT, SIGN, OTA, AO Alliance na Chuo kikuu cha Calfonia San Fransisco Marekani.

Mratibu wa Kongamano la Kimataifa la madaktari Bingwa wa Mifupa Dkt Joseph Mwanga akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kongamano hilo.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Calfonia cha San Francisco, Profesa Michael Terry akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la madaktari wa mifupa duniani.

No comments:

Post a Comment