Thursday, 23 February 2023

Madaktari bingwa wa MOI wapewa mbinu za kisasa za upasuaji wa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo.

 



Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya  na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimeanza kutoa  mafunzo maalum ya upasuaji wa  vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa mbinu za kisasa kwa madaktari bingwa waliohitimu katika chuo hicho ambapo wagonjwa 4 wamefanyiwa upasuaji huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface  amesema mafunzo hayo yanaongozwa na Mkufunzi maalum kutoka hospitali ya St. Luke`s, Ugiriki kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa matibabu ya kibobezi.

“Mafunzo haya ni endelevu ambapo wataalam wetu  watafundishwa upasuaji wa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa mbinu za kisasa  ambapo mpaka sasa wagonjwa wanne kati ya saba waliopangwa wameshafanyiwa upasuaji huo” amesema Dkt. Boniface

Aidha,  Dkt. Boniface ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongwa na Rais  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwani zaidi ya Millioni 50 zimeokolewa kama wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa Ubongo  na  Mishipa ya Fahamu Dkt. Nicephorus  Rutabasibwa amesema Madaktari bingwa watatu wa MOI waliohitimu Chuo cha MUHAS watafundishwa mbinu za kisasa za na za kibobezi zakutibu magonjwa ya  mishipa ya damu kwenye ubongo.

“Mafunzo haya yamegawanyika katika sehemu nne ambapo tunalengo la kuwafanyia wagonjwa  40 katika kipindi cha mwaka mmoja kwa ajili ya  kuwajengea uwezo wataalam wetu ili baadae wawafundishe wenzao waliopo katika hospitali mbalimbali nchini” amesema Dkt. Rutabasibwa

Naye, Mtaalamu Bingwa Mbobezi wa Mishipa ya damu kwenye Ubongo kutoka hospitali ya St. Luke`s kutoka Ugiriki Prof. Athanasios Petridis amesema anafuraha kubwa kuwa MOI na kutoa mafunzo ya kibobezi ya upasuaji wa kuzibua vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo na  baada ya mafunzo hayo wataalam hao watakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji huo.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa Ubongo Dkt. John Michael Mtei  ameushukuru uongozi wa Taasisi ya MOI kwa mafunzo hayo kwani yamewajengea  uwezo  wa kutibu magonjwa ya mishipa ya damu kwenye ubongo .

habari picha na Victoria Stanslaus

No comments:

Post a Comment